Kuandika insha bora ni ujuzi muhimu kwa kila mwanafunzi anayesoma Kiswahili chini ya mfumo wa CBC (Competency Based Curriculum). Iwe wewe ni mwanafunzi wa gredi lolote, kufahamu jinsi ya kuandika insha kwa usahihi kutakusaidia kupata alama za juu na kufaulu mtihani wako.
Katika mwongozo huu, tutakufundisha kila kitu unachohitaji kujua kuhusu kuandika insha bora ya CBC kutoka kwenye muundo, hadi vigezo vya kusahihisha, na vidokezo vya vitendo vya kuboresha uandishi wako.
CBC inaangalia nini kwenye Insha?
Kwa mfano hapa tutangalia nini inatakikana katika insha bora. Kabla ya kuandika, ni muhimu kuelewa vigezo vinavyotumiwa na watahini wa CBC kutathmini insha yako. Tofauti na mifumo ya zamani, CBC inaangalia kwa mfano:
| Kipengele (Criteria) | Maelezo (Description) | Alama (Marks) |
|---|---|---|
| Wazo/Mada | Je, insha ina wazo kuu au mada inayofaa? | 0–4 |
| Mpangilio | Je, insha ina mwanzo, katikati, na mwisho? | 0–3 |
| Lugha na Sarufi | Sarufi, uandishi sahihi, na msamiati unaofaa | 0–4 |
| Ubunifu | Insha ina ubunifu, mawazo mapya, au hadithi ya kuvutia? | 0–3 |
| Uwasilishaji | Uwekaji sahihi wa herufi, mpangilio safi | 0–2 |
| Jumla | 0–16 |
Mfano wa Insha: Mwanafunzi 1
MADA: RAFIKI YANGU
rafiki wangu anaitwa juma yuko shuleni kwangu tunacheza mpira yeye ni mzuri
Uchambuzi wa Alama (Kwa Kigezo cha 20)
| Kipengele | Alama | Maoni |
|---|---|---|
| Wazo/Mada | 1/5 | Wazo lipo (anazungumzia rafiki yake) lakini halijaelezwa kabisa. Sentensi moja pekee. |
| Mpangilio | 0/4 | Hakuna mpangilio kabisa. Haina mwanzo, katikati, wala mwisho. |
| Lugha na Sarufi | 1/5 | Herufi zote ni ndogo. Hakuna nukta wala alama yoyote. Sentensi ndefu mno (ina mawazo mengi katika sentensi moja). |
| Ubunifu | 1/3 | Anataja jina na shughuli, lakini hakuna maelezo zaidi. Mawazo ya kawaida tu. |
| Uwasilishaji | 0/3 | Hakuna mpangilio wowote. Aya hazipo. Mawazo yamechanganyika katika sentensi moja ndefu. |
| JUMLA | 3/20 | Inahitaji kuboreshwa sana |
Jinsi ya kuboresha insha
Moja ya njia muhimu ya kumsaidia mwanafunzi kupata alama zaidi katika insha za CBC ni kuongeza urefu wa maandishi kutoka maneno 200 hadi angalau maneno 400. Insha ndefu humruhusu mwanafunzi kueleza mawazo yake kwa upana zaidi na kutoa maelezo ya kina kuhusu mada aliyopewa.
Kwa mfano, badala ya kusema tu, “Nina marafiki wazuri shuleni,” mwanafunzi anaweza kueleza:
- Marafiki hao wanaitwaje
- Wana tabia gani
- Wanasaidiana vipi
- Wanafanya nini pamoja
Maelezo kama haya huongeza ubunifu, huonyesha umilisi wa lugha, na humruhusu mwanafunzi kutumia msamiati mpana zaidi. Aidha, insha ndefu huwapa walimu nafasi ya kutathmini vizuri sarufi, mpangilio wa mawazo, na uwezo wa mwanafunzi kuelezea hisia na matukio.
Hata hivyo, si urefu pekee unaoleta alama nyingi. Ubora wa maudhui, mpangilio mzuri (mwanzo, kati, mwisho), na matumizi sahihi ya lugha ni mambo muhimu zaidi. Insha yenye maneno mengi lakini yenye makosa mengi ya sarufi inaweza kupata alama chache.
Kwa hivyo, suluhisho bora si kuongeza maneno tu, bali kuongeza maelezo ya maana, ubunifu, na mpangilio mzuri wa mawazo.
Kwa Mfano: insha huu unaweza rekebishwa na kupata alama zaidi ikiwa imeandikishwa bora kama vile
INSHA: RAFIKI YANGU
Rafiki yangu anaitwa Juma. Juma yuko katika shule ninayosoma, na tumekuwa marafiki kwa muda mrefu. Nilimfahamu siku ya kwanza nilipojiunga na shule hii. Alinipokea kwa furaha na kunionyesha maeneo mbalimbali ya shule kama vile maktaba, uwanja wa michezo na darasa letu. Tangu siku hiyo, urafiki wetu umekuwa wa karibu sana.
Juma ni mwanafunzi mwenye bidii darasani. Yeye husikiliza mwalimu kwa makini na hushiriki kujibu maswali. Anapopata kazi ya ziada, huifanya kwa wakati na kwa umakini mkubwa. Mara nyingi hunisaidia kuelewa masomo ninapopata ugumu, hasa katika somo la Hisabati. Tabia yake ya kusaidia wengine humfanya apendwe na wanafunzi wengi.
Zaidi ya hayo, Juma ni mchezaji hodari wa mpira wa miguu. Kila jioni tunapomaliza masomo, huenda uwanjani kucheza mpira pamoja na wanafunzi wengine. Juma ni mzuri sana katika kufunga mabao na kupiga pasi za uhakika. Wakati wa mashindano ya shule, aliwahi kuisaidia timu yetu kushinda kwa kufunga bao la ushindi. Uwezo wake wa kucheza mpira hututia moyo na kutufanya tushirikiane kama timu.
Juma pia ana tabia njema. Ni mnyenyekevu, mwenye heshima na mkweli. Hapendi ugomvi na kila mara huhimiza amani miongoni mwa wenzake. Mimi humheshimu sana kwa sababu ni rafiki wa kweli anayejali na anayesimama nami katika nyakati nzuri na ngumu.
Kwa ujumla, Juma ni rafiki muhimu sana katika maisha yangu ya shule. Urafiki wetu umenifunza umuhimu wa ushirikiano, bidii na kuheshimiana. Ninamshukuru kwa kuwa sehemu ya maisha yangu, na nina matumaini urafiki wetu utaendelea hata tutakapomaliza shule.
Kwa nini Insha hii inaweza kupata 17/20
Mada imeeleweka vizuri na imejikita kwa rafiki mmoja (Juma).
Mpangilio mzuri: mwanzo, kati na mwisho umefuatwa.
Maelezo ya kutosha kuhusu tabia, masomo na michezo.
Sarufi na lugha kwa ujumla ni sahihi.
Inaweza kukosa alama chache kwa sababu haijatumia misemo mingi ya ubunifu au taswira za kina zaidi.
Pia kuna mifano mingine ya upangaji wa alama, lakini iliyo sahihi zaidi kwa insha ni mfumo wa alama 40. Huu ndio unaotoa nafasi pana ya kutathmini vipengele vyote muhimu kama maudhui, mpangilio, sarufi, msamiati na ubunifu kwa kina zaidi. Mfumo wa alama 20 unaweza kutumika katika darasa la chini, lakini alama 40 humwezesha mwalimu kupima uwezo wa mwanafunzi kwa usahihi na kwa undani zaidi. Kwa mfano:
Mada: RAFIKI YANGU
Rafiki yangu wa karibu anaitwa Juma. Tumesoma pamoja katika shule moja tangu nilipojiunga na darasa la nne. Siku ya kwanza nilipofika shuleni, nilihisi upweke kwa sababu sikuwa namfahamu yeyote. Hata hivyo, Juma alinijia kwa tabasamu pana na kunikaribisha kwa maneno ya upole. Tangu siku hiyo, urafiki wetu umekuwa kama mti uliopandwa kandokando ya mto—ukiendelea kukua na kuimarika kila uchao.
Juma ni mwanafunzi mwenye bidii na mwenye malengo maishani. Darasani, husikiliza kwa makini na kuandika dondoo muhimu. Si mtu wa kufanya mzaha wakati wa masomo. Mara nyingi amekuwa akinisaidia kuelewa maswali magumu ya Hisabati na Sayansi. Ana kipaji cha kueleza mambo kwa njia rahisi na ya kuvutia. Kutokana na juhudi zake, amekuwa miongoni mwa wanafunzi wanaofanya vizuri darasani, lakini hajawahi kujivunia mafanikio yake.
Mbali na masomo, Juma ni mchezaji hodari wa mpira wa miguu. Kila jioni, baada ya masomo, hukimbilia uwanjani kwa shauku kubwa. Ustadi wake wa kuumiliki mpira na kupiga mashuti makali huwafanya watazamaji kushangilia kwa furaha. Nakumbuka siku moja tulipokuwa tukicheza dhidi ya shule jirani; timu yetu ilikuwa nyuma kwa bao moja. Dakika za mwisho, Juma alipokea pasi na kupiga shuti la nguvu lililozama wavuni. Bao hilo lilituletea ushindi na furaha isiyoelezeka. Tukio hilo lilinionyesha kuwa Juma si tu mchezaji mzuri bali pia ni kiongozi mwenye ujasiri.
Juma pia ana tabia njema zinazomtofautisha na wengine. Ni mnyenyekevu, mwenye heshima kwa walimu na wanafunzi wenzake, na hupenda kusaidia bila kutarajia malipo. Anahimiza amani na ushirikiano miongoni mwa wenzake. Wakati wowote ninapokumbana na changamoto, hunipa ushauri wa busara na kunitia moyo nisikate tamaa. Kwangu mimi, yeye ni zaidi ya rafiki; ni ndugu niliyempata shuleni.
Kwa ujumla, Juma ni mfano wa kuigwa katika masomo, michezo na maadili mema. Urafiki wetu umenifundisha umuhimu wa bidii, uaminifu na mshikamano. Ninaamini kuwa siku zijazo atafikia ndoto zake kwa sababu ana msingi imara wa tabia na juhudi. Ninamthamini sana na nina matumaini kuwa urafiki wetu utaendelea kudumu hata tutakapomaliza masomo ye
Kwa nini hii inaweza kupata 38–40/40
Maudhui yameelezwa kwa kina
Mpangilio mzuri (mwanzo, kati, mwisho)
Msamiati wa kiwango cha juu (taswira na methali kidogo)
Sarufi sahihi na sentensi zilizokamilika
Ubunifu na mifano halisi